Mchungaji wa Afrika Kusini ambaye miaka miwili iliyopita alivuma kwa kitendo chake cha kuwalisha waumini wake nyoka, panya , na nywele amejitokeza katika kanisa la mhubiri maarufu wa Nigeria, TB Joshua.

Mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mnguni amekaririwa na gazeti la Afrika Kusini la Citizen akidai kuwa moyo wake ulibadilika hasa baada ya kukamatwa na kuachiwa na jeshi la polisi, na kwamba alijisikia kumrudia Mungu wa kweli.

“Nilianza kuangalia Emmanuel TV, kumsikiliza TB Joshua, nikabaini kuwa nilikuwa nafanya kitu ambacho sio cha kiroho. Nilibaini kuwa lile lilikuwa shambulizi dhidi yangu. Nimekuja kwa TB Joshua ili niokolewe,” alisema.
Mnguni alifunguliwa mashtaka na jamii kwa kosa la kufanya ukatili dhidi ya wanyama. Hata hivyo, mashtaka yote yalifutwa baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.