Rais Magufuli amuapisha Aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bibi Anna Mghwira Kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 06 Juni, 2017 amemuapisha Bibi Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro.
Bibi Anna Elisha Mghwira amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Saidi Meck Sadiki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo.
Hafla
ya kuapishwa kwa Bibi Anna Elisha Mghwira imefanyika Ikulu Jijini Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akizungumza
baada ya kumuapisha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Bibi Anna Elisha
Mghwira kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuondoa kero
zinazowakabili wananchi wa Kilimanjaro bila kujali itikadi za vyama vyao
vya siasa, dini, makabilia na kanda wanazotoka.
Mhe.
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa atapata ushirikiano wa kutosha wakati
wote wa utekelezaji wa majukumu yake na asikubali kuyumbishwa na mtu
yeyote katika majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.
“Mimi
huwa siteui watu hivi hivi, huwa naangalia uwezo wa mtu, na wewe
nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia wananchi,
nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro, wapo watu
watakaokusema na wengine watakuonea wivu, wewe kachape kazi” amesema
Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Bibi Anna Elisha Mghwira amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na amemuahidi
kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kujenga
Taifa.
“Ninasema
hii ni heshima kwa Taifa letu, ni heshima kwa umoja wa nchi yetu, ni
heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na minong’ono mingi
sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani, mimi sio
mpinzani wa maendeleo” amesema Bibi Mghwira.
Post a Comment