Tangaza Nasi

Sababu Iliyowafanya Wabunge wa Upinzani Wasuse na kutoka Nje

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika ametolewa nje ya Bunge leo Ijumaa kwa agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Licha ya adhabu hiyo, amemzuia kutohudhuria vikao vya Bunge kwa siku saba kuanzia leo.

Mnyika ametolewa baada ya mmoja wa wabunge kusema 'Mnyika mwizi' akimhusisha na wizi wa madini, hoja inayochangiwa na wengi kwenye mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini unaoendelea.

Kutokana na hali hiyo Mnyika alimtaka Spika kuchukua hatua kwa mbunge aliyesema kuwa yeye ni mwizi lakini Spika akasema hajui hilo na haijaingia kwenye hansadi. Hata hivyo Mnyika alisisitiza kuwa mambo hayaweze kwenda hivyo.

Baada ya majibizano kati yake na Spika, Spika akaamuru walinzi wamtoe Mnyika nje ya Bunge na asihudhurie vikao saba vinavyofuata.

Mnyika alikuwa akitoa maelezo baada ya Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde kusema upinzani wa Tanzania ni wa ajabu kwani unatetea wezi wa madini.
Baada ya hatua hiyo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka nje kupinga mnyika kutolewa nje.

Wakiwa nje ya ukumbi wa bunge, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya alizungumza na waandishi wa habari na kusema hawakubaliani hatua iliyochukuliwa na spika dhidi ya mwenzao kwani kuna mbunge wa CCM alisema wabunge wengine hawana akili lakini hakuchukuliwa hatua yoyote.

“Nadhani hata nyinyi mmeona mbunge aliyekuwa anachangia anasema kuwa wabunge wengine wapimwe akili, inawezekana hawana akili anaachwa kwa sababu tu ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi.”

Aidha, Bulaya alisema kazi ya upinzani ni kuikosoa serikali pale mambo yanapokuwa hayaendi sawa ni si kupongeza kila kitu. Alifafanua zaidi kuwa hawawezi kuwa wanaisifia tu serikali, bali watafanya hivyo pale panapopasa kama kwenye wizara ya ardhi ambapo walimpongeza waziri kwa kazi kubwa anayofanya.

“Msimamo wetu kama Kambi ya Upinzani tumeamua kutoka kwa sababu hatuwezi kujadili mambo ya msingi kwa kufanyiwa mambo haya, sisi kazi yetu ni kuishauri serikali lakini hatuwezi kuishauri serikali vile wanavyotaka wao. Kwenye Wizara ya Ardhi mbona wabunge wa upinzani walisimama na wakapongeza na Wizara ya Ardhi ilipita bila shida yoyote kwa pande zote mbili, sasa kwanini wao wanataka kupongezwa tu? Kazi yetu ni kuona pale ambapo mambo hayaendi sawa kwa mujibu wa sheria tunasema na hili liwe wazi watu waliokuwa wakipigia kelele mikataba mibovu ni upinzani bungeni” alisisitiza Ester Bulaya.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Maadili itamjadili Mbunge Esther Bulaya kwa kosa la kushawishi wenzake kutoka nje.

Spika wa Bunge pia ameiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujadili kitendo cha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee cha kuzuia Askari wa bunge kumtoa nje Mbunge John Mnyika.

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.