Kenya yakumbwa na upungufu mkubwa wa fedha
Wizara ya fedha nchini imekiri kwa serikali inakumbwa na changamoto kubwa za kifedha na haiwezi kabisa kutimiza mahitaji yake.
Ufadhili
wa miradi muhimu ya serikali umeathiriwa zikiwemo serikali za kaunti
ambazo bajeti zao, serikali itazipunguza kwa shilingi bilioni 15 na 17
au dola [147,913,193 na 167,634,953].
Kutokana na ukosefu huo wa
fedha mashirika ya serikali yametakiwa kupunguza matumizi yasiyo ya
lazima na kutumia fedha zilizopo kwa njia inayostahili.
"Kila shirika ni lazima lijizatiti. Tumebuni njia ya kupunguza
matumizi. Tunapunguza matumizi kwa kila sekta ili kwenda sambamba na
fedha zetu," alisema waziri wa fedha Henry Rotich.
Amesema kuwa
hali hii imetokana na kushindwa kwa halmashauri ya ukusanyaji ushuru
nchini Kenya KRA kushindwa kutimiza malengo yake yote ya kukusanya
ushuru na kipindi kirefu cha shughuli za uchaguzi.
"Tumeongea na
KRA Jinsi tunaweza kukabiliana na hilo kupitia ukusanyaji wa kodi ya
ndani na ya nje," Rotich aliiambia Kamati ya ya seneti.
Kulingana
na Rotich serikali inakabiliwa na upungufu wa ukusanyaji ushuru wa
bilioni 70 kwenye makadirio ya serikali ya mwaka 2017/2018.
Kutokana
hilo, kuna uwezekano kuwa wakenya watakumbwa na nyakati ngumu kwa
sababu serikali itaendelea kukopa ndani ikishindana na watu, hali ambayo
itachangia biashara ndogo kuwa na ugumu wa kupata mikopo kutoka kwa
benki.
Hadi Disemba mwaka 2017 deni la Kenya lilikuwa shilingi
trilioni 4.55, deni ambalo limesababisha nchi kutenga asilimia 54 ya
pato lake kulipa madeni.
Maseneta walitaka kujua ni kwa nini
serikali za kaunti hazijapokea fedha kwa miezi minne licha ya seneti
kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo.
Alijibu na kusema kuwa ni
shilingi bilioni 134 tu zimetolewa kwa serikali za kaunti kinyume na
fedha zilizokuwa zikihitajika dola bilioni 302.
CHANZO:BBC

Post a Comment