Rais Mnangagwa amjibu Mugabe; asema Zimbabwe imesonga mbele baada ya utawala wake
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema kuwa, nchi hiyo imeshapiga hatua baada ya kumwondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Robert Mugabe.
Rais wa Zimbabwe amesema hayo akimjibuu Robert Mugabe aliyesema kwamba, hakufikiria kuwa rais wa sasa wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa angemgeuka na kusimama dhidi yake ambapo alilaani pia hatua ya Mnangagwa ya kumuondoa madarakani kwa njia ya mapinduzi.
Katika matamshi yake hayo Mugabe alisema kuwa, "Sikuwahi kufikiria hata siku moja kwamba Emmerson Mnangagwa niliyemlea na kumleta serikalini na ambaye niliokoa maisha yake akiwa gerezani alikotishiwa kunyongwa, kwamba siku moja angenigeuka."
Hata hivyo Rais wa sasa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameyapuuza matamshi hayo ya Mugabe na kusema kuwa, kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe ana haki ya kusema anachotaka kama raia yeyote wa kawaida wa nchi hiyo.
Rais wa Zimbabwe amesema kuwa, taifa hilo limepiga hatua baada ya Mugabe kuondolewa madarakkani na kwamba sasa linasonga mbele likijiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Taifa letu limeshapiga hatua. Lengo letu sasa ni kuandaa Uchaguzi Mkuu mwaka 2018,” amesisitiza Rais Mnangagwa. Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe umepangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Emmerson Mnangagwa, aliyekuwa makamu wa Rais wa Zimbabwe alifutwa kazi na Robert Mugabe na kwenda uhamishoni Afrika Kusini kabla ya kurejea nchini humo na kuchaguliwa na Bunge kuwa rais wa nchi hiyo.
Post a Comment