Morocco kukaguliwa kwa fainali za dunia 2026
Zabuni ya nchi ya Morocco ya kutaka kuandaa fainali za kombe la dunia 2026, itafanyiwa ukaguzi kwa vitendo juma hili kupitia kamati maalum ya shirikisho la duniani FIFA.
Kamati hiyo imeshafika nchini Morocco na inatarajiwa kufanya kazi hiyo kama ilivyofanya katika nchi nyingine zilizoomba uenyeji wa fainali hizo, ambazo ni Marekani, Canada na Mexico.
Shirikisho la soka nchini Morocco limethibitisha kuipokea kamati hiyo yenye watu watano, ambayo itatembelea miji iliyoainishwa katika zabuni ya nchi hiyo, kwa ajili ya kuwa mwenyeji wa michezo ya fainali hizo endapo itafanikiwa kushinda.
Shughuli za ukaguzi nchini Morocco zinatarajiwa kufanywa Aprili 17-19, sambamba na ukaguzi wa viwanja ambavyo vipo tayari tofauti na vile vitakavyojengwa kama nchi hiyo itapata uenyeji.
Jibu la nani atakuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia 2026, linatarajiwa kutoka kupitia mkutano mkuu wa FIFA, ambao umepangwa kufanyika mjini Moscow, Juni 13.
Morocco imewahi kuomba nafasi ya kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mara nne bila mafanikio.
Iliwahi kufanya hivyo kwa ajili ya fainali za mwaka 1994, 1998, 2006 na 2010.
Hata hivyo mwaka 1994 Morocco ilishika nafasi ya pili, ikitanguliwa na Marekani ambayo ilitangazwa kuwa mshindi, mwaka 1998 pia ilishika nafasi ya pili ikitanguliwa na Ufaransa hali kadhalika mwaka 2010 ambapo Afrika kusini walikua wenyeji.
Post a Comment