Lil Wayne, Birdman wakunja makucha, wajipanga upya
Rapa Lil Wayne na Birdman ambao walikuwa na mgogoro mkubwa wa kimkataba na kubadili urafiki wa awali kuwa uhasimu, wamedaiwa kukunja makucha yao na kuingia studio pamoja.
Hivi karibuni, mahakama iliamuru Lil Wayne kuwa huru dhidi ya mkataba wa Cash Money na hivyo kuachia ‘The Carter V’ akiwa kama msanii huru na mmiliki wa lebo ya Young Money baada ya mgogoro wa muda mrefu.
Lakini mtayarishaji wa muziki, D-Roc jana aliibua mapya kwenye Instagram baada ya kuweka picha ya watu wawili wakiwa studio; ingawa ni kwa nyuma, anaonekana Lil Wayne akiwa na rasta zake na mtu aliyekaa ambaye anaonekana kiwiliwili pekee akizibwa sehemu nyingine na Weezy aliyesimama.
‘Like Father Like Son, tunazungumzia vitu ambavyo vipo kiuhalisia #Cashmoney #Youngmoney #SuperEarz #lilwayne #birdman #blatt,” aliandika D-Roc kwa tafsiri isiyo rasmi, kwenye picha hiyo.
Hatua hiyo iliibua hisia kuwa huenda Birdman na Lil Wayne wamerejea kufanya albam ya ‘Like Father, Like Son 2’, ikiwa ni muendelezo wa ile ya kwanza iliyotoka Oktoba 31 mwaka 2006.
Lil Wayne tayari ameshasaini mkataba na Universal Records na amelipwa $10 milioni kwa ajili ya albam yake ya ‘The Carter V’. Albam hiyo imesubiriwa kwa hamu kwa miaka mingi ikicheleweshwa kutokana na mgogoro wa kimkataba kati ya Bosi wa Cash Money, Birdman na Lil Wayne, sasa inaweza kuingia sokoni muda wowote hivi karibuni.
The Carter III ilikuwa albam rasmi ya ‘sita’ (studio albam) ya Lil Wayne iliyotoka Juni 10, mwaka 2008 na kumpa mafanikio makubwa zaidi, akishinda tuzo nzito ya Grammy ya Albam Bora ya Mwaka. Alikabidhiwa tuzo hiyo mwaka 2009.
Leo, Weezy anasherehekea miaka takribani 10 tangu kutoa ‘The Carter III’.
Post a Comment