Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma imemuhukumu kunyongwa hadi
kufa mtu mmoja aitwaye Kinyota Kabwe mkazi wa Muzye wilayani Kasulu kwa
kosa la kumuua kwa makusudi jirani yake kwa kumchoma mkuki mara tatu na
kusingizia alikuwa amechanganyikiwa.
Kesi hiyo namba 105 ya Jamhuri dhidi ya Kinyota
Kabwe imesikilizwa na Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo Lameck Mlacha,
inaelezwa mnamo Septemba 15, 2013 majira ya saa tisa alasiri mshtakiwa
akiwa na mkuki alienda nyumbani kwa Lucia Tekena na kumchoma mkuki
shingoni,kifuani na tumboni huku binti wa marehemu nae akijeruhiwa na
mshtakiwa.
Inaelezwa kabla ya tukio hilo ambalo baada ya muda
mfupi mwanamke huyo alipoteza maisha na yeye kukamatwa nikama kulikuwa
na ugomvi na mvutano kati yake na mkewe nyumbani kwake ambao unahisiwa
kuna uwezekano ulikuwa una muhusisha marehemu pia hivyo kusababisha
mauaji hayo.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili Antia Julius
na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Edna Aloyce. Upande wa utetezi
uliwasilisha ushahidi wa mshtakiwa na kaka yake ulio eleza mshtakiwa
ana matatizo ya akili na alikuwa anatumia dawa kwa muda hivyo kuna
wakati hali ilikuwa inakuwa mbaya huku muhusika akisema hakumbuki tukio
la kuchoma mkuki.
Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano akiwemo aliye
shuhudia mauaji hayo na Daktari wa magonjwa ya akili aliye mpima na
majibu yakawa kuwa hana ugonjwa wowote wa akili. Jaji Mlacha amesema
inaonyesha mshtakiwa alikusudia kuua ndio maana alielekeza mkuki tumboni
,kifuani na shingoni na suala la ugonjwa wa akili hiyo ni namna ya
kutafuta kujitetea na haina mashiko, hivyo akamhukumu adhabu kunyongwa
hadi kufa.
Post a Comment