Tangaza Nasi

Watu 16 wameuawa katika shambulizi dhidi ya kituo cha kijeshi nchini Burkina Faso

 

Takriban wanajeshi 12 na raia wanne waliojitolea kushirikiana na jeshi waliuawa Ijumaa ya jana katika shambulio lililolenga kituo cha jeshi Kaskazini mwa Burkina Faso.

Taarifa ya jeshi imesema shambulizi hilo lililenga kikosi cha jeshi cha Namissiguima katika mkoa wa Sanmatenga, eneo la Centre-Nord, mwendo wa saa tano asubuhi.

Taarifa hiyo imesema idadi ya awali inaonyesha wanajeshi 12 na askari wa kujitolea wanne wameuawa, huku askari wengine 21 wakijeruhiwa. Jeshi la Burkina Faso limetuma vikosi vya kuimarisha usalama zaidi katika eneo hilo.

Eneo la Kaskazini mwa Burkina Faso limekuwa likishuhudia mashambulizi ya kigaidi tangu 2015, ambapo zaidi ya watu 1,000 wameuawa na zaidi ya milioni 1 kukimbia makazi yao.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi inatawaliwa na wanajeshi tangu Januari kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Roch Kabore.

Kiongozi wa kijeshi, Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba ametangaza usalama kama moja ya vipaumbele vyake. Hata hivyo kuongezeka kwa mashambulizi kumeripotiwa katika wiki za hivi karibuni.

                                     Wanajeshi wa Burkina Faso wakiwa katika mazoezi

Hivi karibuni wananchi wa Burkina Faso walifanya maandamano ya kushinikiza kuhitimishwa uhusiano na ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi yao na Ufaransa.

Maandamano hayo yaliitishwa na muungano wa vyama vya kiraia nchini humo ambao umeitaka serikali mpya ya mpito nchini humo kusimamisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi na Ufaransa. Waburkinabe wanasema licha ya kuwepo askari wa Ufaransa nchini humo, magaidi bado wanaendeleza mashambulizi dhidi ya raia na jeshi.

Muungano huo unaojulikana kama Unification Bureau sambamba na kutaka kukatwa uhusiano wa kijeshi na nchi hiyo ya Ulaya, lakini pia umesisitiza kuwa, unafadhilisha ushirikiano wa nchi yao na Russia katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi.


 

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.