Tangaza Nasi

Reli mpya ya kisasa yazinduliwa nchini Kenya kuunganisha miji ya Mombasa na Nairobi


media                                "Reli mpya inayopitra katika reli ya kati kutoka Mombasa kwenda jijini Nairobi"
Reli ya kisasa imezinduliwa nchini Kenya kuunganisha jiji Kuu Nairobi na mji wa Pwani Mombasa, kusafirisha abiria zaidi ya elfu Moja na mizigo umbali wa Kilomita 485 kwa  muda  wa kati ya saa nne na tano kati ya miji hiyo miwili.

Uzinduzi umefanyika mjini Mombasa na kuongozwa na rais Uhuru Kenyatta na wawakilishi wa serikali ya China, ambao walisafiri kutumia treni hiyo iliyopewa jina Madaraka Express, kwenda jijini Nairobi.

Ujenzi wa reli hii umeigharimu serikali ya Kenya Dola Bilioni 3.2 kwa msaada wa mkopo kutoka China.

Inakuwa reli ya kwanza ya kisasa kujengwa baada ya ile ya wakoloni kutoka Uingereza iliyojengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Rais Kenyatta amesema reli hii  inawaunganisha wakenya na ni hatua ya kihistoria.
“Nawaomba Wakenya wote waweke kando tofauti zao za kisiasa, ukabila na kusherehekea mafanikio haya makubwa,” alisema rais Kenyatta.

Aidha, rais Kenyatta ametoa onyo kali kwa wale watakaokamatwa na kupatikana na makosa ya kuharibu vifaa vya reli hii mpya watapewa adhabu ya kunyongwa.
“Wale watakaokamatwa kwa kuharibu mali ya umma, mali ya Wakenya na kuthibitishwa kufanya makosa hayo, nitatia saini wanyongwe, " alisisistiza rais Kenyatta.
 
                                                  Kituo chaabiria mjini Mombasa
Usimamizi wa reli hii mpya na safari za treni zitasimamiwa na watalaam kutoka China kwa muda wa miaka mitano kabla ya kuikabidhi serikali ya Kenya.

Uzinduzi huu umekuja wakati huu nchi hiyo ikitarajiwa kuwa na Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti. Wachambuzi wa siasa wanasema rais Kenyatta ametumia uzinduzi huu kujipigia debe ili kuchaguliwa tena.

Hatua ya Kenya inatoa matumaini ya ukanda wa Afrika Mashariki kuunganishwa na reli ya kisasa kwa ajili ya kuboresha usafiri na biashara katika eneo hilo.

Reli ya kati inatarajiwa kuunganisha mataifa ya Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Tanzania na Ethiopia katika siku zijazo. Tanzania tayari imezindua ujenzi wa reli yake kutoka jijini Dar es salaam kwenda mjini Morogoro.
  
                              " Treni la mizigo kutoka Mombasa hadi Nairobi ilivyozinduliwa Mei 30 2017"
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa maswala ya uchumi nchini humo na hata Benki ya dunia, iliitaka Kenya kuboresha reli yake ya  zamani badala ya kujenga reli mpya kwa sababu itagharimu fedha nyingi.

Upinzani nchini humo pia  umekuwa ukihoji kiasi kikubwa cha fedha kilichotumiwa katika mradi huo, na hatua ya serikali ya rais Kenyatta kufuta mkataba uliokuwa umeafikiwa katika serikali iliyopita.

Wakati uo huo, serikali ya Kenya imeanza mazungumzo mengine na serikali ya China kufadhili mwendelezo wa ujenzi wareli hiyo kutoka Nairobi kwenda mjini Kisumu karibu na mpaka wa Uganda, kwa kima cha Dola Bilioni 3.5.

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.