Akaunti 88 za Rais Jammeh Zafungwa, Waziri wa Serikali Mpya Adai Alikwapua Dola Milioni 50..!!!
WAZIRI wa Sheria wa Gambia, Abubacarr Tambadou, amesema kiongozi wa
zamani wa nchi hiyo, Yahya Jammeh, ameiba kiasi cha dola za Marekani
milioni 50 kutoka katika kampuni ya mawasiliano ya taifa hilo na tayari
mahakama imetoa amri ya kutaifisha mali zake.
“Rais Yahya Jammeh yeye binafsi au kwa kutoa maelekezo mahsusi amekwapua
dola za Marekani zisizopungua milioni 50,” anasema waziri huyo na
kuongeza; “..Jumatatu (Novemba 22, 2017) tumepata amri ya mahakama
kuhusu kutaifisha mali zake au kuzizuia.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, hii ni mara ya kwanza kwa
serikali mpya ya taifa hilo kutoa maelezo rasmi kuhusu wizi alioufanya
rais huyo wa zamani aliyeongoza taifa hilo kwa miaka takriban 22
mfululizo.
Waziri Tambadou aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mahakama ya nchi
hiyo imeamuru kufungwa kwa akaunti takriban 88 zenye jina la Jammeh
katika benki mbalimbali, sambamba na ‘kuzishikilia’ kampuni 14
zinazohusishwa na mkuu huyo wa nchi wa zamani.
Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh alizaliwa Mei 25 mwaka 1965, ni
mwanasiasa aliyetokea katika jeshi na alianza kuiongoza Gambia kuanzia
mwaka 1994 hadi 2017, akiwa mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Kijeshi
(AFPRC) na baadaye kuwa rais wa nchi hiyo kuanzia 1996 hadi 2017.
Post a Comment