Azam wataweza kuishi wanachokiamini?
Azam FC imeanza kuboresha kikosi chake baada ya leo Juni 5, 2017 kuingia mkataba na mshambuliaji Waziri Junior kutoka Toto Africans ambayo imeshuka daraja, kwa mujibu wa website ya timu hiyo, Junior alipendekezwa na kocha mkuu Aristica Cioaba na amekuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Azam.
Junior alikuwa straika kinara wa Toto Africans ya Mwanza msimu uliopita, akiwa mfungaji wao bora kwa mabao sita aliyofunga.
Azam wamewapa nafasi vijana wengi kutoka kikosi cha vijana na usajili wa mchezaji wao wa kwanza ni mzawa kwa hiyo unaanza kuona wanauvaa uhalisia katika uendesha wa klabu.
Abbas Kapombe, Abdul Haji, Godfrey Elias, Ramadhan Mohamed na kiungo Stanslaus Ladislaus ni wachezaji ambao wamepandishwa kwenye kikosi cha kwanza kutoka timu ya vijana.
Wadau inabidi wawape muda Azam kwa sababu Azam imeamua kuja na aina mpya ya uendeshaji wa klabu yao kwa kuwatumia wachezaji wanaowalea wenyewe huku wakitumia kiasi kidogo cha pesa katika usajili.
Hawajaanza kupata pesa za kutosha zinazotokana na vyanzo vya klabu kwa hiyo unaweza kuhoji pesa nyingi wanazotumia katika usajili wanazitoa wapi? Hapo ndipo kwa wenzetu Ulaya wanakutana na rungu la Financial Fair Play.
Endapo vilabu vingine vya Tanzania vitafuata nyayo za Azam katika mfumo wao mpya walioamua kuja nao, kuna kitu kikibwa tutavuna baada ya muda.
Ukiangalia timu kama Mbao FC imeweza kufanya iliyoyafanya msimu uliopita huku ikiwa na bajeti ndogo tu, kila mtu anaijua historia ya Mbao kwamba ilipewa taarifa ya kucheza ligi kuu siku chache kabla ya msimu kuanza.
Wakasajili vijana ambao hawakuwa na majina makubwa hapo kabla wakawajenga ili kupambana na moto waliouwasha msimu uliopita kila mmoja ameuona na kuvutiwa na timu hii changa kwenye soka la Tanzania.
Kwa hiyo watu wameanza kuvutiwa kwamba, inawezekana kuwekeza kwa vijana ikiwa watajengwa vizuri na kuaminiwa.
Lakini kikubwa ni suala la malengo ya klabu, kila klabu ina malengo yake na tamaduni zake iliyojiwekea yenyewe. Kuna klabu ambazo malengo yao ni kuzalisha wachezaji na kuwauza huku ikihakikisha haishuki daraja na wala haipambani kupata ubingwa. Kuna klabu ambazo ndoto zao za kila siku ni kunyanyua ‘makwapa’ hapa utazitaja Simba, Yanga pamoja na Azam.
Sasa kama Azam wataamua kuchukua ubingwa isiwe kipaumbele chao kwa kuamua kuwatengeneza vijana wao wenyewe, kuwamini na kuwapa nafasi ili badae washindane bila kutumia gharama kubwa kwa kusajili wachezaji wa bei mbaya na kuwalipa mishahara mikubwa.
Mtego kwa Azam ni kwamba, Je, wako tayari kucheza bila presha ya ubingwa? Hapa ndipo inakuja tofauti kati ya Mbao na wao kwa sababu Mbao wanacheza wakiwa hawawazi ubingwa wanachokifanya wao ni kutengeneza timu na kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi nzuri, kama ubingwa ikitokea wamepata kama ilivyokuwa kwa Leicester City basi ni jambo jema.
Post a Comment