Tangaza Nasi

Kenya yaadhimisha miaka 53 ya uhuru wa bendera


 media

Kenya inaadhimisha miaka 53, tangu ilipopata uhuru wa bendera kutoka kwa wakoloni wa Uingereza, ambao walikubali kuwa nchi hiyo inaweza kujitawala na kuahidi kuipa uhuru wa Jamhuri  tarehe 12 mwezi Desemba mwaka 1963.
Ni siku ambayo wakenya wanakumbuka harakati za vuguvugu la Mau Mau, lililoongozwa na Dedan Kimathi, lilivyopambana na wakoloni kudai uhuru  wa nchi hiyo  makabiliano yaliyodumu kati ya mwaka 1952-1960.
Rais Uhuru Kenyatta ataongoza maadhimisho ya sikukuu hii inayofahamika kama Madaraka, katika Kaunti ya Nyeri nje ya jiji la Nairobi.
Hii ndio sikukuu ya kitaifa ya mwisho nchini humo kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 8 mwezi wa nane.
Maadhimisho ya mwaka huu pia yanahudhuriwa na mgombea wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga kama ishara ya mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki, inajivunia maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa nchi ya kidemokrasia yenye vyama vingi ikiwa ni pamoja na kuongoza kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais Kenyatta anatarajiwa kuwaeleza wananchi wa taifa  hilo mafanikio ya serikali yake kwa muda wa miaka minne iliyopita lakini pia kuhimiza uchaguzi wa amani, huru na haki.
Kupanda kwa gharama ya maisha, kashfa za ufisadi na changamoto za kiusalama kutokana na  mashambulizi ya kigaidi ya Al Shabab kutoka Somalia ni baadhi ya changamoto ambazo yameendelea kuiandama serikali ya rais Kenyatta.
Ni maadhimisho yanayokuja siku moja baada ya rais Kenyatta kuzindua reli mpya ya kati na treni la mwendo kasi kutoka mjini Mombasa kwenda jiji kuu la Nairobi, kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo.

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.