Mahakama kutoa uamuzi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais Kenya
Mahakama ya rufaa nchini Kenya tarehe 23 mwezi huu
itatoa uamuzi kuhusu ikiwa matokeo ya urais yatakayotangazwa katika
maeneo ya bunge ndio yatakayokuwaya mwisho au yanaweza kutathminiwa upya
na Tume ya Uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi ilikata rufaa baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa matokeo yanayotangazwa katika maeneo ya bunge yawe ya mwisho, lakini Tume inadai kuwa hali hiyo inaweza kuzua hitilafu.
Muungano wa upinzani NASA, unataka uamuzi wa Mahakama kuu usibadilishwe na umetishia kutoshiriki katika uchaguzi wa mwezi Agosti ikiwa uamuzi huo utabadilishwa kwa madai kuwa, unaweza kuzua udanganyifu wakati wa kujumuisha matokeo ya mwisho.
Wakili wa upinzani James Orengo amewaambia kuna uwezekano mkubwa wa matokeo ya mwisho kubadilishwa na Tume ya Uchaguzi ikiwa, matokeo kutoka maeneo bunge hayataheshimiwa.
Mwanasheria Mkuu wa serikali Githu Muigai na Mawakili wa Tume ya Uchaguzi wamewaambia Majaji wa Mahakama hiyo kuwa, Mwenyekiti wa Tume ambaye kwa sasa ni Wafula Chebukati amepewa mamlaka ya kutangaza matokeo ya mwisho ya urais.
Upinzani pia wamesema matokeo ya urais yanaweza kubadilishwa na Mahakama kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo na sio kupitia Tume ya Uchaguzi.
Majaji Asike Makhandia, Kathurima M'inoti, Patrick Kiage, William Ouko na Agnes Murgor, ndio wanaosikiliza kesi hiyo wakati huu kampeni za kisiasa zikiendelea kushika kasi.
Wachambuzi wa siasa wanasema Majaji hao wana jukumu la kutoa uamuzi utakaoridhisha pande zote za kisiasa na kwa mujibu wa sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Agosti.
Post a Comment