Asilimia 98 ya wapiga kura wa upinzani nchini Venezuela wapinga mabadiliko ya katiba

Wapiga kura Milioni saba wengi wao wafuasi wa upinzani wamepiga kura nchini Venezuela, kupinga mpango wa serikali wa kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo na kumpa mamlaka makubwa rais.
Rais Nicholas Maduro amesema kura
hiyo ya maoni haina maana yoyote huku matokeo yakionesha kuwa asilimia
98 ya waliopiga kura, wamepinga katiba kufanyiwa marekebisho.
Wapiga kura pia wanataka Uchaguzi mpya kuitishwa nchini humo na
kuondolewa madarakani kwa rais Maduro ambaye wapinzani wanasema ni
dikteta.
Wakati uo huo, watu waliokuwa na silaha wakiwa juu ya pikipiki
wamempiga risasi na kumuua mpiga kura wa upinzani nchini Venezuela
wakati akiwa katika mstari wa kupiga kura ya maoni.
Imebainika kuwa mtu aliyepigwa risasi ni mwanamke mwenye umri wa
miaka 61 ambaye ni Nesi aliyekuwa anajiandaa kushiriki katika zoezi hilo
lisilotambuliwa na serikali.
Mbali na kifo hicho, watu wengine watatu wamejeruhiwa katika shambulizi hili na wanapewa matibabu.
Msemaji wa upinzani Carlos Ocariz amesema mauaji ya mwanamke huyo
yamewapa hasira na uchungu baada ya wafuasi wao 100 kupoteza maisha
katika makabiliano na maafisa wa usalama kuanzia mwezi Aprili.
Kura hii ya maoni inakuja wakati huu serikali ikiandaa kura ya maoni
itakayofanyika tarehe 30 mwezi huu, ili kuibadilisha katiba hiyo.

Post a Comment