Makamu wa Rais Samia Suluhu awa Mlezi wa Girl Guides
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewahimiza wazazi na walezi nchini
kuwalea vijana wao katika maadili mema ili waje kuwa viongozi au raia
wema ambao watakaoliletea taifa tija na sifa ya uongozi bora.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
ametoa maelekezo hayo katika hafla ya kukabidhiwa kuwa mlezi wa Tanzania
Girl Guides Association (TGGA) kutoka kwa mlezi anayemaliza muda wake
Mama Salma Kikwete katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es
Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amesema ili kazi ya kujenga maadili mema iweze kufanyika vizuri nchini
ni muhimu kwa wananchi wote kuunga mkono jitihada zinafanywa na Serikali
kwa sasa za kupambana na watu wanaovuruga maadili ya Kitanzania ili
tabia hiyo iweze kukomeshwa haraka.
Amesema kuwa Serikali imejipanga ili
kuhakikisha rasilimali zinazopatikana nchini zinanufaisha wananchi wote
wakiwemo vijana wa kike na wa kiume.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amekipongeza Chama cha Tanzania Girl Guides Association kwa jitihada
zake za kueneza misingi na stadi za kuishi kwa uadilifu,uzalendo kwani
kufanya hivyo wanajenga taifa lenye watu waadilifu.
Makamu wa Rais pia ameuhakikishia uongozi
wa chama hicho kuwa atakuwa nao bega kwa bega katika kuhakikisha chama
hicho kinajiendesha kwa faida bila kutegemea wafadhili ambao wanazidi
kupungua kila uchao.
“Niwaombeni mbuni mbinu mpya za
kujiongezea kipato ili kuwaongezea uwezo wa kujiendesha, mbinu hizo ni
kama kutumia ardhi mliyonayo kwa kukopa benki au kuingia ubia na
makampuni yaliyo tayari kushirikiana nanyi ili muweze kujenga majengo
yenu ambayo mtaweza kupangisha na kupata kodi ambazo mtaweza
kujiendesha, kujiongezea kipato na kuendesha chama kwa tija na ufanisi
zaidi”. Amesisitiza Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mlezi wa Chama cha
Tanzania Girl Guides Association aliyemaliza muda wake Mama Salma
Kikwete amesema katika kipindi cha uongozi wake chama hicho kimeweza
kuongeza idadi ya wanachama kutoka 97,000 mwaka 2015 hadi zaidi ya
wanachama 100,000 kwa sasa na jitihada hizo bado zinaendelea.
Mama Salam amesema anaimani kuwa chini ya
uongozi wa mlezi mpya Mhe Samia Suluhu Hassan chama hicho kitafanya
kazi vizuri zaidi katika kuwalea vijana wa kike katika maadili mema ili
waweze kujiepusha na vitendo vibaya katika jamii ikiwemo matumizi ya
dawa za kulevya.

Post a Comment