Mapacha walioungana wafaulu kidato cha sita
Pacha walioungana, Maria na
Consolata wamejawa na furaha baada ya kufaulu mitihani yao ya mwisho ya
kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa,
Kusini magharibi mwa Tanzania.
Maria na Consolata, walio na umri
wa miaka 19, wamefaulu kwa kupata daraja la pili katika masomo yao ya
kidato cha sita na kuwa na matumaini kuwa ndoto yao ya kuwa walimu hapo
baadaye inaelekea kutimia.
Maria na Consolata wameieleza BBC furaha yao:
"Tulipokea
matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na
shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya
vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya
mwisho huwezi kujiamini sana," ameeleza Consolata.
Mabinti hawa wangependa kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu Cha Ruaha mkoani humo.
Wameeleza
sababu za kuchagua chuo kwenye mkoa wanaoishi tofauti na vyuo vingine
au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao wangependa kubadili
mazingira.
"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka
kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na
walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa
mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo
hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali
hii tumeizoea.''
Maria na Consolata wanaona kuwa, hakuna linaloshindikana iwapo wazazi watawajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu
"
Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione
kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na
kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya
kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.''


Post a Comment