Tutaendelea kuvifungia vituo vya mafuta
Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya
............................................................................................................................
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa licha ya kufungia mamia ya
vituo vya mafuta nchi nzima, leo itaendelea na operesheni hiyo ya
kufunga vituo vingine vya mafuta ambavyo havijafunga moja kwa moja
mashine za malipo za kielektroniki (EFDs) na pampu.
Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya amesema kuwa
waliofungiwa vituo vyao vya mafuta, watafunguliwa tu iwapo watakidhi
vigezo ambavyo ni pamoja na kulipia mashine na kuingia makubaliano na
mamlaka na TRA.
“Tunatoa mwito kwa wale ambao tumeshawafungia wafuate vigezo
ili waweze kufunguliwa, wakalipie na waingie na makubaliano na TRA mkoa
kwamba ni lini watafunga mashine baada ya kuzilipia,”, amesema Mwandumbya.
Mwandumbya amesisitiza kuwa kwa sasa TRA haitaruhusu wenye vituo vya
mafuta waendelee kutumia mashine za mkono ambazo ziko nje ya Pampu kwani
wametumia mwanya huo kwa muda mrefu kukwepa kodi ya serikali.
“Kamwe hatutaruhusu wafanyabiashara waendelee kukwepa kodi
kwa kisingizio cha wananchi kuteseka kwa kukosa huduma, tunachotaka
wafuate sheria ya kufunga mashine za EFDs kwenye vituo vyao”.
Akifafanua ulipaji uliokuwa unatumika awali Mwandumbya amesema kati
ya watu 10 waliokuwa wakijaza mafuta ni wawili tu ndio waliokuwa
wanapewa risiti tena kwa kuzidai.
Hata hivyo TRA inaendelea na operesheni ya kukagua na kufungia vituo
vya mafuta vinavyoendelea kukaidi agizo hilo la kununua na kufunga
mashine za EFDs.
“Kwa Dar es Salaam peke yake tumeshafungia vituo 71, leo
tunacompile (tunakusanya) takwimu za nchi nzima na tutatoa taarifa kwa
vyombo vya habari,”amesema Mwandumbya.
Chanzo:HabariLEO


Post a Comment