Mabaki mwili wa mwanafunzi aliyepotea siku 250 yapatikana
Mabaki ya mwili wa mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya sekondari Ikuti Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Levis Mwailemele (16) yamepatikana katika pori la msitu Nkisyo.
Mwanafunzi huyo alipotea katika mazingira tata, Januari 9, 2022 na mabaki yake yamepatikana Septemba 18 ikiwa ni siku 252.
Mabaki hayo ni pamoja na fuvu la kichwa, mifupa na nguo ambazo zimepatikana katika pori hilo.
Baada ya kupatikana kwa mwili wa mwanafunzi huyo, ndugu wa marehemu walifuata taratibu za kisheria na kuendelea na shughuli za mazishi makaburi yaliyopo kijiji cha Lyenje kata ya Ikuti wilayani humo.
Imeelezwa marehemu alikuwa akiishi na bibi yake na kwamba mara ya mwisho ilikuwa siku ya Jumapili alikwenda kanisani na tangu alipotoa saa 6.00 mchana hakurejea tena nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili, bibi wa marehemu, Queen Asubisye alisema mjukuu wake alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kutoka kanisani akirejea nyumbani.
''Kama ilivyo kawaida yake, mjukuu wangu alikuwa anapenda sana kusali alienda kanisani na kuhudhuria ibada mara baada ya ibada hakurejea tena licha ya juhudi za kumtafuta kushindikana mpaka tulipo ukuta mwili na nguo alizovaa mara ya mwisho,'' alisema
Ndugu wa Marehemu, Edward Mwambaghi alisema walipata taarifa kuwepo kwa mwili wa mtu katika msitu wa pori la Nkisyo ndipo walifutilia na kubaini ni mtoto wao aliyetoweka.
''Marehemu alitoweka katika mazingira ya kutatanisha sana na tumefanya kila jitihada za kumtafuta bila mafanikio mpaka tulipoukuta mwili wake ikiwepo fuvu la kichwa na nguo zake,'' alisema.
Alisema katika uhai wake, marehemu alikuwa na maendeleo mazuri shuleni na kuishi vizuri na jamii iliyomzunguka na hivyo kama familia wameumizwa na tukio hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lyenje, Kata ya Ikuti wilayani Rungwe, Chuo Mwakasege alisema hawezi kuzungumzia lolote kuhusiana na tukio hilo kwani analiachia Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzunga alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alisema yupo nje ya mkoa na kwamba atalifuatilia na kujua uhalisia wa tukio na kutoa taarifa
Akizungumza kwa masharti ya kutoandikwa jina gazetini, mkazi wa kata ya Ikuti alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwa watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na kukutwa mabaki ya miili yao huku akiiomba Serikali kutoa elimu kwa jamii kupinga matukio hayo wakiwepo wazee wa mila (machifu).
VIA: MWANANCHI
Post a Comment