Tangaza Nasi

Fahamu kwanini Waziri wa Utalii Zanzibar amejiuzulu

 

"Simai Mohammed Said, aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)"
 
Siku moja kabla ya kujiuzulu, Simai Mohammed Said, aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alikutana na wawekezaji na wadau kutoka jumuiya tofauti kutafuta suluhisho la upungufu wa vileo.

Januari 24, 2024 Simai aliilalamikia Bodi ya Vileo kubadilisha mawakala wa kuingiza vinywaji Zanzibar.

Kupitia video iliyosambaa mitandaoni usiku wa kuamkia leo Januari 26, 2024 Simai alitangaza amejiuzulu kutokana na alichodai mazingira yasiyo rafiki ya kazi.

Simai ambaye pia ni mwakilishi wa Tunguu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), katika taarifa aliyorekodiwa kwenye picha jongefu (video) amesema: "Nimeandika barua ya kujiuzulu nafasi yangu kuanzia leo (jana Januari 25, 2024). Nimefikia uamuzi huu ambao si rahisi katika utamaduni wetu.”

“Kutokana na hilo jukumu namba moja la wasaidizi wa Rais ni kumsaidia kutekeleza ilani na inapotokea mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo la ustawi wa wananchi, ni vyema kutafuta jawabu kwa haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea hata ikibidi kukaa pembeni," amesema.

Amesema amefikia uamuzi huo mgumu wa kukaa pembeni.

Simai katika kikao cha Januari 24, 2024 alizungumzia upungufu wa vileo, kabla ya kukutana na wawekezaji na wadau kutoka jumuiya tofauti kwa ajili ya kutafuta suluhisho.

Alisema majadiliano na wadau ndiyo yatawezesha Serikali kuboresha maeneo yenye tatizo ili kuchochea utalii na uchumi wa Zanzibar.

Amesema sekta hiyo ikinyooshewa kidole kidogo basi athari zake ni kubwa, kwani tayari Zanzibar imeshajifunza nyuma katika matukio tofauti na haitaki kurudi huko.

Amebainisha mara nyingi amekuwa akikaa pamoja na mawaziri wenzake kuona wanaliweka sawa jambo hilo na kuhakikisha sekta hiyo haisuisui.

“Masikitiko yamekuwa makubwa na imenibidi niitishe kikao, kwani Serikali na mimi tumeshaanza kunyooshewa vidole na wadau na hili siwezi kulikalia kimya, kwani wawekezaji na watalii ni wadau muhimu kwetu,” amesema.

Sekta ya utalii pekee inachangia zaidi ya asilimia 30 katika uchumi wa Zanzibar.

Aliwaomba wadau wa sekta ya utalii na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuendelea kuwa wavumilivu, huku Serikali ikilitafutia ufumbuzi jambo hilo.

Kikao hicho pia amesema kililenga kuangalia mwaka mpya wa sekta hiyo na changamoto zinazojitokeza kwani utalii ni suala mtambuka.

"Simai Mohammed Said, aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakati akiapishwa kushika nafasi hiyo kabla ya kujiuzulu"

Simai ni nani?

Simai kabla ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 2015, alikuwa mfanyabiashara aliyejikita zaidi katika sekta ya utalii.

Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati), pia mjumbe wa bodi ya chama hicho.

Ni miongoni mwa waanzilishi wa Tamasha la Sauti za Busara na amewahi kuwa mwenyekiti wa tamasha hilo.

Mwaka 2015 baada ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi, mwaka 2018 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.

Baadaye mwaka 2020, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alimteua kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (Wema), kabla ya kumuhamishia Wizara ya Utalii, Machi 22, 2022.

Chanzo: Mwananchi

 

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.