Tangaza Nasi

Ajib Ataka Milioni 60 Asaini Singida United..!!!

KIUNGO Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, amewataka Singida United kumpa Sh milioni 60 ili wapate saini yake kwa ajili ya kuwatumikia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ajib ambaye kaonyesha nia ya kuondoka Simba baada ya mkataba wake kuisha na kwenda kutafuta changamoto nyingine ya soka, jina lake limetajwa na kocha Hans Pluijm kwenye kikosi chake.
Tayari mchezaji huyo amekwishaweka bayana kuwa anahitaji fedha hizo na endapo itashindikana, hawezi kujiunga na timu hiyo mpya kwenye Ligi Kuu msimu ujao.
Mbali na Ajib pia timu hiyo imeonyesha nia ya kumtaka mchezaji wa Yanga, Deus Kaseke ambaye naye anahitaji Sh milioni 40.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Singida United, Festo Sanga, alithibitisha kufanya mazungumzo na wachezaji hao, lakini bado hawajafikia hatua ya kuwafanya wasaini katika klabu hiyo.
“Ni kweli tunawahitaji na tumefanya nao mazungumzo na tumeweka wazi kiasi ambacho tunacho mkononi, ila inaonekana wao bado hawapo tayari, hivyo tunawasubiri  wao wakiwa tayari sisi hatuna shida muda wowote wakitufuata tutasaini,” alisema Sanga.
Alisema kuwa malengo yao msimu huu ni kusajili wachezaji 25, wapya wakiwa 14, saba kutoka nje na saba wengine kutoka ndani, huku mpaka sasa wachezaji wa ndani bado watatu kwa kuwa wamesajili wawili tu.

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.