Tanzania yabadilisha uamuzi wake wa kuondoa marufuku ya kusafirisha nje wanyamapori
Serikali ya Tanzania imetangaza kubadilisha uamuzi wake wa kuondoa marufuku yenye utata ya kusafirisha wanyamapori nje ya nchi.
Tangazo hilo la kubadilisha uamuzi huo limekuja siku moja tu baada ya hatua hiyo kuzua malalamiko mengi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Marufuku ya kusafirisha wanyamapori nje ya nchi iliwekwa mwaka 2016, ili kulinda wanyama na ndege wanaolindwa nchini humo ambao walikuwa wakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.
Hata hivyo juzi Jumamosi, mamlaka ya wanyamapori nchini Tanzania ilitangaza kuwa, ingeondoa marufuku hiyo kwa muda wa miezi sita kuanzia Jumatatu ya leo tarehe 6 Juni hadi tarehe 5 Disemba mwaka huu kwa wafanyabiashara kuondoa “akiba ya wanyama” ambao hawakuweza kuwauza kwa sababu ya marufuku hiyo.
Hata hivyo Pindi Chana Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangaza kurejesha marufuku hiyo ili kuruhusu mashauriano zaidi.
Waziri Pindi amenukuliwa na duru za habari akisema kuwa, “Kulikuwa tangazo ambalo linaruhusu usafirishaji wa wanyamapori nje ya nchi, lakini kama waziri mhusika, nimesimamisha hatua hiyo mara moja,”.
Uamuzi wa kuondoa marufuku ya kusafirishha wanyamapori nje ya nchi ulizua ukosoaji na malalamiko makubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku Watanzania wengi wakitaka upitiwe upya.
Tanzania inafahamika kwa fukwe zake za kuvutia katika visiwa vya Zanzibar,lakini pia matembezi ya safari ya kutazama wanyama pori pamoja na mlima mrefu barani Afrika,Kilimanjaro,yote hayo yakiwa vivutio vikubwa kwa watalii.
Post a Comment